John 8

Mwanamke Aliyefumaniwa Akizini

1 aLakini Isa akaenda katika Mlima wa Mizeituni. 2 bAlfajiri na mapema Isa akaja tena Hekaluni, watu wote wakakusanyika, akakaa akaanza kuwafundisha. 3Walimu wa sheria na Mafarisayo wakamleta mwanamke mmoja aliyefumaniwa akizini. Wakamsimamisha katikati ya umati wa watu wote. 4Wakamwambia Isa, “Mwalimu, huyu mwanamke amekutwa akizini. 5 cKatika sheria, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake wa namna hii, mpaka wafe. Sasa wewe wasemaje?” 6 dWalimuuliza swali hili kama mtego ili wapate sababu ya kumshtaki.

Lakini Isa akainama akaanza kuandika ardhini kwa kidole chake.
7 eWalipoendelea kumuulizauliza akainuka, akawaambia, “Kama kuna mtu yeyote miongoni mwenu ambaye hana dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe.” 8Akainama tena na kuandika ardhini.

9 fWaliposikia haya, wakaanza kuondoka mmoja mmoja, wakianzia wazee, hadi Isa akabaki peke yake na yule mwanamke akiwa amesimama mbele yake. 10Isa akainuka na kumwambia, “Wako wapi wale waliokuwa wanakuhukumu kuwa mwenye hatia?”

11 gYule mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja Bwana.”

Isa akamwambia, “Hata mimi sikuhukumu. Nenda zako, kuanzia sasa usitende dhambi tena.”]

Isa Nuru Ya Ulimwengu

12 hKisha Isa akasema nao tena akawaambia, “Mimi ni nuru ya ulimwengu. Mtu yeyote akinifuata hatatembea gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”

13 iMafarisayo wakamwambia, “Ushuhuda wako haukubaliki kwa kuwa unajishuhudia mwenyewe.”

14 jIsa akawajibu, “Hata kama najishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ni kweli kwa sababu najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda. 15 kNinyi mnahukumu kwa kufuata vipimo vya kibinadamu, mimi simhukumu mtu yeyote. 16 lLakini hata kama nikihukumu, uamuzi wangu ni sahihi kwa sababu sitoi hukumu yangu peke yangu, bali niko pamoja na Baba, aliyenituma. 17Imeandikwa katika Sheria yenu kwamba, ushahidi wa watu wawili ni thabiti. 18 mMimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma hunishuhudia.”

19 nNdipo wakamuuliza, “Huyo Baba yako yuko wapi?”

Isa akawajibu, “Ninyi hamnifahamu mimi ni nani, wala hammfahamu Baba yangu. Kama mngenifahamu mimi, mngemfahamu na Baba yangu.”
20 oIsa alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika chumba cha hazina Hekaluni. Lakini hakuna mtu aliyemkamata kwa kuwa saa yake ilikuwa haijawadia.

Isa Atabiri Kifo Chake Mwenyewe

21 pIsa akawaambia tena, “Ninaenda zangu, nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi ninyi hamwezi kuja.”

22 qNdipo wale Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Je, hii ndiyo sababu amesema, ‘Niendako mimi ninyi hamwezi kuja’?”

23 rAkawaambia, “Ninyi mmetoka chini, mimi nimetoka juu. Ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. 24 sNiliwaambia kuwa mtakufa katika dhambi zenu, kwa maana msipoamini ya kwamba ‘Mimi Ndiye,’ mtakufa katika dhambi zenu.”

25 tWakamuuliza, “Wewe ni nani?”

Naye Isa akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nimekuwa nikiwaambia tangu mwanzo.
26 uNina mambo mengi ya kusema juu yenu na mengi ya kuwahukumu. Lakini yeye aliyenituma ni wa kweli, nami nanena na ulimwengu niliyoyasikia kutoka kwake.”

27Hawakuelewa kuwa alikuwa akiwaambia juu ya Baba yake wa Mbinguni. 28 vKisha Isa akawaambia, “Mtakapokwisha kumwinua juu Mwana wa Adamu, ndipo mtakapojua kuwa, ‘Mimi ndiye yule niliyesema na kwamba mimi sitendi jambo lolote peke yangu bali ninasema yale tu ambayo Baba yangu amenifundisha. 29 wYeye aliyenituma yu pamoja nami, hajaniacha, kwa kuwa siku zote nafanya mapenzi yake.’ ” 30 xWengi waliomsikia Isa akisema maneno haya wakamwamini.

Wanafunzi Wa Kweli

31 yKisha Isa akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkidumu katika maneno yangu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli. 32 zNdipo mtaijua kweli nayo kweli itawaweka huru.”

33 aaWao wakamjibu, “Sisi tu wazao wa Ibrahimu, nasi hatujawa watumwa wa mtu yeyote. Wawezaje kusema kwamba tutawekwa huru?”

34 abIsa akajibu, “Amin, amin nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. 35 acMtumwa hakai nyumbani anakotumika siku zote, lakini mwana hukaa nyumbani daima. 36 adHivyo Mwana akiwaweka huru mtakuwa huru kweli kweli. 37 aeNinajua ya kuwa ninyi ni wazao wa Ibrahimu, lakini mnatafuta wasaa wa kuniua kwa sababu ndani yenu hamna nafasi ya neno langu. 38 afNinasema yale niliyoyaona mbele za Baba yangu, nanyi inawapa kufanya yale mliyosikia kutoka kwa baba yenu.”

Isa Na Ibrahimu

39 agWakajibu, “Baba yetu ni Ibrahimu.”

Isa akawaambia, “Kama mngekuwa wazao wa Ibrahimu mngefanya mambo yale aliyofanya Ibrahimu.
40 ahLakini sasa ninyi mnatafuta kuniua, mtu ambaye nimewaambia kweli ile niliyosikia kutoka kwa Mungu, Ibrahimu hakufanya jambo la namna hii. 41 aiNinyi mnafanya mambo afanyayo baba yenu.”

Wakamjibu, “Sisi hatukuzaliwa kwa uzinzi. Tunaye Baba mmoja, Mungu pekee.”

42 ajIsa akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda, kwa maana nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, ila yeye alinituma. 43 akKwa nini hamwelewi ninayowaambia? Ni kwa sababu hamwezi kusikia nisemacho. 44 alNinyi ni watoto wa baba yenu ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli maana hamna kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo. 45 amLakini kwa sababu nimewaambia kweli hamkuniamini! 46 anJe, kuna yeyote miongoni mwenu awezaye kunithibitisha kuwa mwenye dhambi? Kama nawaambia yaliyo kweli, mbona hamniamini? 47 aoYeye atokaye kwa Mungu husikia kile Mungu asemacho. Sababu ya ninyi kutosikia ni kwa kuwa hamtokani na Mungu.”

Maelezo Ya Isa Kuhusu Yeye Mwenyewe

48 apWayahudi wakamjibu Isa, “Je, hatuko sahihi tunaposema ya kwamba wewe ni Msamaria na ya kwamba una pepo mchafu?”

49Isa akawajibu, “Mimi sina pepo mchafu, bali ninamheshimu Baba yangu, nanyi mnanidharau. 50 aqLakini mimi sitafuti utukufu wangu mwenyewe, bali yuko anayetaka kunitukuza, naye ndiye mwamuzi. 51 arAmin, amin nawaambia, mtu yeyote akilitii neno langu hataona mauti milele.”

52 asNdipo Wayahudi wakamwambia, “Sasa tumejua kwamba una pepo mchafu. Ikiwa Ibrahimu alikufa na vivyo hivyo manabii, nawe unasema, ‘Mtu akitii neno langu hatakufa milele.’ 53 atJe, wewe ni mkuu kuliko baba yetu Ibrahimu ambaye alikufa na manabii ambao nao pia walikufa? Hivi wewe unajifanya kuwa nani?”

54 auIsa akawajibu, “Kama nikijitukuza utukufu wangu hauna maana. Baba yangu, huyo ambaye ninyi mnadai kuwa ni Mungu wenu, ndiye anitukuzaye mimi. 55 avIngawa hamkumjua, mimi ninamjua. Kama ningesema simjui, ningekuwa mwongo kama ninyi, lakini mimi ninamjua na ninalitii neno lake. 56 awBaba yenu Ibrahimu alishangilia kwamba angaliiona siku yangu, naye akaiona na akafurahi.”

57Wayahudi wakamwambia, “Wewe hujatimiza hata miaka hamsini, wewe wasema umemwona Ibrahimu?”

58 axIsa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, kabla Ibrahimu hajakuwako, ‘Mimi niko.’ ” 59 ayNdipo wakaokota mawe ili kumpiga, lakini Isa akajificha, naye akatoka Hekaluni.
Copyright information for SwhKC